Na Jackline
Masinde
Geita/Nyang’hwale: Huu nimsiba usiyofutika!!!
Ni maneno
ambayo nimeona pengine yanafaa kuelezea tukio la familia ya Watoto wenye ulemavu wa ngozi,
Lemy Juma (12) Zakharia Juma (6) waliotekwa na majambazi miaka nane iliyopita.
Tukio hilo
liliacha simanzi isiyofutika kwa familia ya Lemy na Zakharia ambao walitekwa na
majambazi nyumbani kwao saa 2:00 usiku 14 Augosti 2007, wakiwa kwenye maandalizi
ya chakula cha Jioni,huko kijiji cha Buhalahala kata ya Kalangalala wilaya ya
Geita .
Ikiwa bado
Taifa linahuzunika juu ya Kifo cha Yohana Bahati(1) mkazi wa kijiji cha ilelema
aliyetekwa na majambazi mikononi mwa mama yake kisha kuuawa kikatili kwa
kukatwa miguu na mikono yake miwili na kiwiliwili chake kutupwa katika shamba
la mahindi huko hifadhi ya Bihalamulo wilayani Chato.
Pia tukio la
Mtoto Pendo Emmanuel aliyetekwa na watu wasiyojulikana na kutokomea
kusikojulikana ambae hadi leo hajapatikana,mtoto mwingine Baraka cosmas(6)
huko wilaya ya Sumbawanga ,ambae alikatwa mkono wake wa kulia na watu
wasiyojulikana .
Matukio
hayo,yaliamsha hisia za waliowengi,huku wengi wakijiuliza nani anafanya matukio
haya,kwanini albino wanatekwa na kuuawa,wanaohusika je wanakamatwa?.
Matukio haya
yananikumbusha tukio la kwanza kutokea katika wilaya ya Geita la mtoto Lemy na
Zackharia waliotekwa hadi leo
hawajulikani walipo na hakuna mtu yeyeote aliyekamatwa na hakuna juhudi
zozote zilizochukuliwa dhidi ya tukio hilo.
Najiuliza
sipati jibu,watoto hawa wako wapi mpaka sasa.Je? wako hai,nani alihusika na
tukio hilo.Je ?hatua gani zimechukuliwa kuhakikisha watoto hawa wanapatikana?.Je?
kwanini sijasikia kelele kama ilivyo kwa tukio la Pendo Yohana na wengine?.
Majibu ya
maswali haya yananipa utata ndipo nilipoamua kufatilia mkasa huu mwanzo hadi
ulipoishia,hivyo nilifunga safari kwenda nyumbani kwa wazazi wa watoto hawa,nikiamini
ndiyo wanaweza kunipa majibu yaliyosahihi.
Ni safari
ndefu sana,yenye misukosuko ya ubovu wa barabara,iliyoanza saa 2:48 asubuhi kutoka
Geita mjini kuelekea kitongoji cha Nyangombe kijiji cha Nyashilanga Wilaya ya
Nyang’hwale mkoani Geita ilipo familia hiyo kwasasa.
.
Nilivuka
mapori na mapori,nilivuka vichaka vya kutisha,nilivuka mito na milima hatimae niliwasili
nyumbani kwa mzee Katemi Shigata babu yake na watoto hao saa 11:40 jioni.
Hakika
nilichoka sana,kwani ilikuwa safari ya kuunga unga kutokana na shida ya usafiri
katika wilaya hiyo.Jua nalo lilikuwa linaishilia,giza lilikuwa limeanza kutokea
kwa mbali.
Ni familia
kubwa yenye watu zaidi ya 40 wanaoishi sehemu mmoja,kwamaana baba na mama,
watoto,wajukuu,vitukuu,ndugu na jamaa.
Niliona
wakiwa wamekaa katika makundi,wengine walionekana wakikusanya kuni za kukoka
moto wa kikome,wengine waliingiza ngombe zizini,wengine walionekana wakipasua
kuni.Hakika walikuwa katika maandalizi ya jioni.
Nilikaribishwa
na wanafamilia hao ambao walionekana kupigwa na butwaa baada ya kuniona huku
wakiwa na shahuku ya kutaka kujua mimi ninani na ninashida gani.
“Karibu
dada!(mwandishi)nilipewa kigoda cha kukalia.
Walijawa na
hofu kubwa, wengi waliamini ni askari nimekuja kuwakamata.
“Dada wewe
ninani,siku hizi tunaogopa tukiona watu tu tunajua ni mapolisi wa serikali
wanakamata watu”alisema mmoja wa wananfamilia hao huku akinikagua kwa macho.
Nilijitambulisha
kwao,na kuwaeleza kilichonileta,wengi walionekana kutoniamini kabisa na badala yake
walinihoji maswali yanayohusu jeshi la polisi.
“Hivi dada (mwandishi)
hawa maaskari wanaokamata waganga wakienyeji wanatumia utafiti gani kuwajua kama
ndiyo wanasababisha mauaji ya albino,maana wanakamata tu watu hata kama siyo
mganga?alihoji Kulwa Shigata mmoja wa wanafamilia hao.
Inanipa kazi
ngumu kubadilisha mtazamo wao kama mimi
ni raia mwema kwao,ilinibidi nitumie taaluma yangu kuwaleta kwenye mstari, lakini
mwisho walinielewa ndipo niliwaleta kwenye mada iliyonileta kwao.
Niliona
walijikusanya ,waliokuwa wamesimama walitafuta mahali pa kukaa,waliokuwa mbali
waliitana na kuakaa .
Maskini! Bila
kujua nilihamsha uzuni na majonzi upya kwa familia hii,mara wote walionekana
kukaa kimya kwa muda wa dakika 2,huku mmoja wa wananfamilia hao ambae baadae niligundua ni mama mzazi wa
watoto hao Mihayo Shigata akishindwa kujizuhia na kuanza kulia.
“Wanangu
jamani...,nilikuwa nimesahau....,sijui wako wapi,Lemy na Zackharia mko wapi...?,mliondoka
mkiwa wadogo sana sasa hivi mmekuwa wakubwa wanagu”alilia kwa uchungu Mama
huyo.
Ooh Mungu wangu!Baba mzazi Juma Charles nae anashindwa kujizuhia,yeye analia huku
akitupia lawama Jeshi la Polisi .
Polisi!!polisi!!
wanajali watu wenye pesa...nakumbuka nilito taarifa polisi wakaniambia
nikatafute mwenyewe nikiwapata nitawajulisha,Wanangu mko wapi?”alihoji kwa
uchungu.
Ilikuwa
ngumu kujizuhia,uchungu wa wazazi hawa ulinifanya pia nidondoshe chozi,lakini
nilijikaza na kuanza kuwatuliza wanafamilia hawa.
“Jamani hebu
tulieni tumweleze,labda tutasaidiwa kuwapata watoto wetu”alisema Charles.
“Dada
umeturudishia majonzi tena,tulishasahau haya mambo,mimi siwezi kueleza
vizuri,ongea na baba mzazi wa hawa watoto”alisema Katemi Shigata babu wa watoto
hao.
Simulizi inaanza.
Inamchukua
muda wa dakika tano akilia,huku baba yake Katemi akimbembeleza asilie,”nyamaza
mwanangu wewe ni mtoto wakiume jikaze,umsimulie huyu mwandishi labda tutapata
msaada wa kuwapata wajukuu wangu”alimtuliza mwanae.
“Ilikuwa ni
mwezi Agosti (alianza kusimulia)mwaka 2007 tarehe sikumbuki majira ya saa 2:00
usiku tukiwa tumekaa nje tukisubiri chakula cha Jioni,ghafla walikuja watu
watano wakiwa wamevaa kininja(wamefunika uso wao ) huku wamevalia makoti
meusi”Charles.
Charles
alieleza alisikia watu hao wakiwa na
mapanga wakiwaambia wachuchumae chini na wajifunike uso wao usionekane huku
wakigonganisha panga zao.
Niliogopa
sana,kwani vitu hivyo havijawahi kunitokea katika maisha yangu,nimekuwa nikisia
tu kwingine”alisema .
“Walituambia
tulale kifudifudi na tujifunike nguo,tulitii amri,licha yakuwa mimi sikuwa na
nguo ya kujifunika,moja ya jambazi hao alinikanyag kichwani ili nisiweze
kunyanyauo uso wangu”alisema.
Alisema
walipigwa ovyo ovyo na majambazi hao kwa kutumia bapa za panga,huku wakiwaamuru
wasipige kelele.
Sikujua
lengo la ujio wao hao majambazi, nikiwa nimekanyagwa kichwa nilijiuliza
kimoyomoyo hawa watu wanataka nini,mbona mimi ni mtu maskini sina kitu
chochote”alijiuliza baba huyo.
Alisema
hakuwaza moyoni kama majambazi hao walikuwa na lengo la kuchukua watoto
wake,wazo lake halikuwepo kabisa na kwa kipindi hicho kesi za albino hazikuwepo
hivyo hilo lilikuwa tukio la kwanza kutokea kwa wilaya ya Geita.
Wakati
nikijiuliza hayo nilisikia wakimlazimisha mke wangu aonyeshe walipo
watoto,kwani wakati wanatuvamia watoto walikuwa ndani wamelala wanangu
watatu,wawili walikuwa albino na moja hakuwa albino.
“Wewe watoto
wako wapi,tuonyeshe watoto wako wapi”aliwanukuu ,walimpiga mke wangu ,ndipo
majambazi hayo yaliingia ndani na kuanza kutafuta watoto.
“Waliwachukua
watoto wote watatu na kuwalaza kifudifudi,lakini nilisikia mmoja wa majambazi
hao akiwaelekeza wenzao kuwa hao wawili wawekeni huku.”alisema .
Wakati
wakitupiga vibaya na mapanga yao nilisikia watoto wakikimbia ,ambapo majambazi
hao walisema kamata hao watoto wanakimbia’kumbe hiyo ilikuwa ni mchezo tu
kusema watoto wanakimbia kumbe ndiyo waliwachukua na kuondoka nao”alisema.
Alisema
sikuelewa kitu niliona kama maigizo,baada ya muda niliona kimya na jambazi
lililokuwa limeniganyaka liliacha kunikanyaga ila niliona mwanga mkali wa
tochi.
Sikutaka
kunyanyuka kuona kwani nilihisi bado wapo kumbe walikuwa wameondoka ila
waliacha tochi kubwa ikiwaka.
Alisema
iliwachukua muda wa nusu saa wakiwa wamelela kifudifudi licha ya ukimya mkubwa
kutawala,hakujua kama watoto wamechukuliwa.
“Nilinyanyua
kichwa change taratibu nakuangaza kuona kama wameondoka,niliona kweupe tu zaidi
ya hiyo tochi na mke wangu na dada yangu niliyekuwa naishi nae wakiwa
wamelala”alisimulia baba huyo.
Alisema
aliwaamsha na kuanza kupiga kelele,wakiomba msaada,wakati huo hawakuwaza kama
watoto wao wamechukuliwa kwani waliamini wapo, labda wamekimbilia nyumba za
jirani.
“Walikuja
watu wakakusanyika majirani wa karibu,tukaweleza yaliyojiri,tuliamua kulala
baada ya kuona kumetulia,na tukauliza walipo watoto tukaambiwa wapo kwa
jirani”alisimulia.
“Usiku huo
haukuwa na amani tena,ulijawa hofu kubwa,sikulala kabisa usiku huo,asubuhi
kulipo kucha tuliwafatilia watoto ,tukampata mmoja Masumbuko Juma(17) ambae
hakuwa albino”alieleza.
Alimuuliza
mwane waliko wenzake lakini alijibu kuwa
wakati wanakimbia alikimbia na kaka yake
Remi na Zakharia lakini walikamatwa na majambazi hayo yeye akakimbia na
kujificha kichakani.
Majibu ya
mwanae yalimpa mashaka na kuanza kujiuliza sasa watoto wako wapi,na wakati huo
hakuwa na wazo kama walichukuliwa na majambazi hao ila siku zilivyozidi kwenda
na matukio ya kuuawa albino ndipo alipoanza kuamini kuwa uwenda wale majambazi
ndiyo walichukua watoto wao.
“Nilianza kuwatafuta watoto hao kwenye nyumba za
majirani lakini hatukuwapata”alisema.
Alisema
waliamua kutoa taarifa kituo cha Polisi Geita juu ya watoto hao kupotea,Polisi
waliwaambia waendelee kutafuta wakiwapata watawajulisha.
“Zilipita
siku mbili bila mafanikio,wala kusikia fununu,tulizunguka kila kona ya kijiji
na mitaa yote hatukuwapata,tulirudisha taarifa polisi,walikuja eneo la tukio na
kufanya uchunguzi kisha kufungua jarada namba GE/IR/2688/2007”alisema.
Waliendelea
kutafuta maeneo yote ya Geita,walikuwa waanasikia fununu sehemu fulanani
amepatikana albino,wakienda kufatilia wanakuta siyo watoto wao.
"Polisi baada
ya kufungua jarada hilo hawakuendelea tena ,walikaa kimya tukaamua kuendelea kutafuta
wenyewe lakini mpaka leo hii saa na dakika hii ninayoongea sijui watoto wangu
wako hai,nani aliwachukua”alisema.
Anasema
wakati huo alijua watoto wake walipotea tu kawaida,lakini kadri siku
zilivyozidi matukio hayo yaliongezeka,ambapo baada ya tukio la watoto wake
lilifata tukio la Zawadi Magindu mkazi wa kijiji cha Nyamaruru ambae alivamiwa
na kukatwa miguu na mkono mmoja .
“Tukio hilo
liliniogopesha na kuanza kujiuliza tena ,hueanda na wanangu wameshakatwa viungo
,kwasasbabu siko nao karibu,sijui waliko ,tulianza upya kuwatafuta kwa hofu ya
watoto wangu kuuawa lakini bado haikuzaa matunda”alisema .
Alisema
walikaa tena wakasikia tukio la albino wengine 6 walikatwa mikono,vidole na
wengine kunyolewa nywele zao,matukio hayo pia yalizidi kumuumiza moyo.
Baada ya
hapo mpaka sasa hivi nikajua kumbe hata wanangu walikuwa kwenye kundi la
maalbino wanaotekwa na kuuawa kisha kuchukuliwa viungo vyao,baada ya matukio
haya kuongezeka na kutangazwa kila siku.
Masumbuko asimulia .
Masumbuko
ambae kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka
10,anasimulia jinsi majambazi hayo walivyoingia ndani na kuwakuta
wamelala.
"Tulikuwa
tumelala tukasikia nje kunakelele ,tukastuka mimi na Fikiri na Zakharia,wakati
huo Lemy alikuwa nje na mama,ghafla majambazi wawili wakaingia ndani na
kumchukua Fikiri ,na Zakharia mimi nikajimbaza nyuma ya mlango”alisema.
Alisema
alitoka nje kwa kunyata na kukimbia nyumba ya Jirani yao Bahati India alipofika
aliwaambia nyumbani kunamajambazi.
Nilipowaambia
wote tukakimbia kwenda kujificha,na India akakimbia nyumba zingine za jirani
kuwaambia ili wapige mwano”alisema
Alisema
baada ya hapo hakujua nini kilichoendelea kwani alilala kwa jirani hakurudi
nyumbani hadi kesho yake.
Alisema
kesho yake asubuhi alipofika nyumbani
kwao alikuta watu wengi.”Baba akaniuliza kaka na mdogo wagu wako wapi?
,nikawambia sijui waliko mimi nilikimbia peke yangu.
Alisema baada
ya kueleza hayao alisikia ndugu zake walipotea ,watu wakaanza kuwatafuta lakini
hawakuonekana hadi leo.
"Najisikia
huzuni sana ,kwani sijui ndugu zangu wako wapi,nani aliwachukua,wapo hai au
wamekufa?”alihoji mtoto huyo huku akishindwa kujizuhia na kuangusha machozi.
Mama mzazi wa watoto anena ya moyoni.
Baada ya
kuongea na mume wake na mtoto wake ,nilimgeukia mama ambae kiukweli alitia
huruma,sikutaka kumuumiza lakini ilinibidi tu nifanye nae mahojiano ili
kukamilisha taaluma yangu.
Kinachoniuma
dada,(mwandishi) wanawake wenzangu ambao watoto wao wamefanyiwa ukatili
wamesaidiwa na serikali,walau hata kupata mwili wa mtoto Yohana Bahati,bora
mama huyo hata analiona kaburi la mwane”alilalamika.
“Mimi
nilieje?Bora wangewakata hata viungo vyao kama alivyokatwa mtoto Baraka
Cosmas(6) na kumwacha “alilia mama huyo.
Mama
alieleza hisia zake huku akitokwa na machozi yasiyokauka,kuwa Serikali isaidie
kuwatafuta watoto wake ,licha yakuwa hajui kama wako hai.
“Sijui wanangu
waliwaua...!sijui walikatwa tu viungo wakawaacha?!,sijui walitupwa maporini
kama Yohana wakafia huko, mimi sijui Mungu Wangu!!”alilalamika mama kwa
uchungu.
Aliendelea
kulalamika mama huyo mwenye nzao 10 huku kati ya hizo nzao tatu ni za watoto
wenye albinisim ambao ni Lemy ,Zakharia na Marko Juma(6) ambae kwa sasa
analelewa na kituo cha watoto wenye albinism mwanza.
Alisema Lemy
ndiye mwanae wa kwanza huku Zakharia ni mtoto wa tatu na Pendo ni mwane wa
saba,anasema kwa sasa amebakia na watoto saba ambapo wawili ambao ni Albino
walitekwa na majambazi huku mtoto wake mwingine ambae siyo albino alikufa kwa
ugonjwa tu wakawaida.
Hakika ni
msiba usiyofutika kwa mama huyu na familia nzima ya watoto hawa,huku swali lao
kuu likiwa ni wapi walipo watoto wao,nani aliwateka,je wako hai au
wamekufa,wamekufa kifo gani,kama wapo hai wanaishi wapi na nani anaishi nao?.
Ndugu na jamaa wanena.
Shigata ni
babu wa watoto Zakharia na Lemy ambae aliamua kukusanya watoto wake wote wakike
na wakiume na kukaa nao nyumbani kwake.
Alisema
baada ya tukio hilo kutokea na matukio hayo yakaendelea kuwepo hapa Geita ,na
mwanae tena akazaa mtoto mwenye Albino aliamua kuwaambia waje kuishi kwake
kulinda usalama wa mjukuu wake Marko Juma(6).
“ waliondoka
Buhalahala mwaka 2009 nakuja kuishi kwangu,lakini baadae tukafanya utaratibu wa
kumpeleka mtoto Marko kituo cha watoto wenye albino Mwanza kulinda usalama wake”alieleza
Shigata.
Kwilabya Shigata,ni
mama mdogo wa watoto hao,anakiri kuwepo kwa tukio hilo,nay eye nimoja wa
mashuhuda wakuu watukio.
“Yaani
siwezi kuielezea siku hiyo,ndoo gete(hapana kabisa),nilijikojolea siku hiyo
mimi na ukubwa wangu niliokuwa nao,sikia kwa mtu mwingine tu”alisema Dada huyo
huku akikataa kabisa kuvuta kumbukumbu ya tukio hilo.
Viongozi wa kijiji cha Nyashilanga.
Hakika
nilikamilisha mahojiano na wanafamilia hao,licha yakuwa ilikuwa kazi ngumu sana
kwangu,na giza nalo lilikuwa limeingia,kwani ilitimia saa 1:30 usiku.
Nilimuita
Dereva aliyenibeba ,ili kuanza safari yakurudi makao makuu ya wilaya ya
Nyang’hwale,ni umbali mrefu zaidi ya saa moja nanusu kwa usafiri wa pikipiki.
Tayari
nilijawa na hofu mimi na dereva aliyenibeba,kwani kijiji cha Nyashilanga
kilikuwa na giza nene,na mapori makubwa,lakini tulikaza moyo.
Dakika 10 zilikuwa zimepita kufika makoa makuu ya
Kijiji tulikutana na ofisa mtendaji wa kijiji Saidi Ndekwa senta ya kijiji hicho.Tulitumia dakika 5
kuzungumza nae juu ya familia ya watoto waliotekwa.
“Hilo tukio
nililisikia,na familia hiyo tunaifahamu kama viongozi wa kijiji kwamba walikuwa
na watoto watatu wenye Albino,wawili walitekwa na majambazi na mmoja alipelekwa
mwanza kwaajiri ya usalama”alisema Ndekwa.
Alisema
wazazi wa watoto hawa walikuwa wakiishi kijiji cha Buhalalahala kitongoji cha
Ishinde,ambako ndiko watoto wao walipotelea ,baadae ndiyo wakaja kuishi hapa
kwa mzee Katemi ambae ni mzee wa kijiji
hiki kwani ni watoto wake.
Baada ya
maongezi hayo ilikuwa imetimia saa 1:45
usiku,tuliendelea na safari ya kwenda makao makuu ya wilaya,kwaajiri ya
kupunzika.
Ohh! Mungu nimkubwa!nilifika
mjini Nyang’hwale saa 2:30 usiku,nikiwa salama.
Mashahidi wa tukio hilo kijiji cha Buhalahala
Asubuhi
Safari ya kurudi Geita ilianza saa 12:00 kutokana na uchovu niliokuwa
nao,niliamua kupumzika siku mzima.
Kesho yake
nilifunga safari kuelekea kitongoji cha Ishinde Kijiji cha Buhalahala kata ya
Kalangalala kilometa 10 tu kutoka Geita mjini
ambako tukio la kutekwa watoto hao lilikotokea.Lengo lakuja hapa
nikuwatafuta mashahidi walioshuhudia tukio hilo.
Moja kwamoja
nafikia ofisi ya Kijiji (ambayo kwasasa ni ofisi ya mtaa), nilikutana na
mtendaji wa mtaa huo Mathias Mbassa na kumweleza kilichonileta,alionekana kuwa
mgeni wa tukio hilo ndipo alipomtafuta mwenyekiti wa kijijiThomas Mageni.
Mmh!umesema
lilitokea lini?hebu ngoja nimpigie Mwenyekiti”alisema huku akichukua simu yake
mfukoni (alianza kutafuta namba kwenye simu).
Hallo!
Mwenyekiti hebu njoo ofisini hapa mara moja”alikata simu na kunisihi nisubiri
dakika chache.
Dakika
chache Kadhaa aliwasili Mwenyekiti huyo,alielezwa na mtendaji nilichomweleza
kisha kunitambulisha kwake.
“Hilo tukio
nalikumbuka kulikuwa na familia mmoja ilikuwa na watoto albino wawili walipotea
usiku baada ya kuvamiwa na majambazi na wakati huo mimi nilikuwa mwenyekiti wa
kijiji hiki”alisema huku akivuta kumbukumbu.
Ndiyo..nimekumbuka
mama,ulikuwa unasemaje sasa?aliniuliza mwenyekiti huyo,nikamweleza yaliyoyangu.
Alisema
tukio la kutekwa kwa watoto hao alilipata kesho yake Asubuhi baada ya kupigiwa
simu na mwenyekiti wa kitongoji husika.
Nilienda
eneo la tukio na kuanza kupiga mwano kuwakusanya wananchi wote,ikabidi tutoe
taarifa polisi juu ya watoto kupotea na kuvamiwa na majambazi.
Alisema
Polisi ilibidi wamkamate baba mzazi wa watoto hao ,kwa kosa la tukio kutokea
usiku na kuamua kulala badala ya kupiga yowe ili watoto watafutwe.
“Baba huyo
alikuwa hawezi kujieleza ilibidi akamatwe na polisi kuwa ameuza watoto wake
,kwanini hakupiga yowe usiku huo”alisema na kuongeza baada ya kukamatwa baba
huyo muda mfupi tulimuona ameachiwa sisi tukajua labda ameonekana hana
hatia”alieleza.
Alisema
baada ya hapo sikuona tena chochote na hao watoto hawakuonekana hadi leo.
Baada ya
maelezo ya mwenyekiti tulitembea Kilometa 2 kwenda nyumbani ilikokuwa familia
hiyo,kweli tulikuta hakuna nyumba watu walishahama,kumegeuka mashamba nasiyo
makazi tena.
Zilionekana
Nyumba jirani na eneo hilo mita 300,tulienda katika nyumba hizo nakukuta watoto
wakicheza,tuliwauliza walipo wakubwa,hawakutuelewa kwani hawakujua Kiswahili.
Wakubwa zenu
wako wapi?aliwahuliza mwenyekiti kwa lugha ya kisukuma,walimjibu ‘alemomunumba
omayo’(mama yuko ndani),walimuita mama yao.
Mama
huyo ambae alikuwa mrefu na mtu mwenye
miraba mine,alitoka nje huku akionekana anafuta machozi kwenye macho yake,hii
ilionyesha alikuwa anapika ndani.
Alisalimia,kwa
Lugha ya kisukuma,hakika mama alikuwa mchangamfu ajabu,alileta viti tukakaa.
Hakujua
Kiswahili hivyo aliongea kisukuma mwanzo mwisho,nilimuuliza juu ya tukio la
watoto Albino waliotekwa,alionekana kuwa mwenyeji wa tukio hilo na kusema na
lifahamu lakini mimi hapa ni mgeni nilikuja mwaka juzi,labda kwa mzee Bahati
India.
Tulikwenda
kwa mzee India ambae ndiye Shuhuda namba moja aliyeletewa taarifa na Mtoto
Masumbuko muda mfupi tu baada ya majambazi hao kuvamia.
“Hapa
anasimulia..”ilikuwa saa 3 hivi,alikuja mtoto anakimbia huku analia,akatuambia
nyumbani kwao wamevamiwa na majambazi”alisema.
Alieleza
kuwa taarifa hizo ziliwastua familia nzima ,ambapo kila mmoja aliogopa na
kukimbia ovyo ili kujificha.
Nilikimbia
kwa jirani yangu Edward Kulwa nikamweleza kwa jirani yetu wamevamiwa,tulianza
kupiga yowe ili kujikusanya twende eneo la tukio tukiwa wengi”alisema.
Alisema
walipofika nyumbani kwa Charles walikuta majambazi wameondoka,wakamwambia
mwenye mji wapige kelele ili watu waje mwenye mji akakataa na kuwaambia
wakalale kwani majambazi wameshaondoka.
"Tulirudi
kulala kila mtu,asubuhi kulipokucha ndipo ikaonekana watoto wawili
hawaonekani,tukaaanza kupiga mwano ili kuwatafuta watoto lakini hawakuonekana
hadi leo”alisema India.
Uongozi wa walemavu wanena.
Baada ya
kujiridhisha na mashuhuda hao,nilimtafuta mwenyekiti wa Chama cha Walemavu mkoa
wa Geita Isack Timothy eye alinipa orodha ya matukio ya watu wenye ulemavu wa
ngozi waliokwisha kutekwa kujeruhiwa na wengine kuuawa.
"Nakubali
kwenye orodha yetu tunao watoto wawiliwa familia moja ambao walitekwa hadi leo hawajaonekana,tukio
hili halikupewa uzito wowote na hata jeshi la polisi halikufatilia hadi
leo”alisemaTimoth.
Pia albino
watatu kwa wilaya ya Geita,na mmoja kutoka wilaya ya Chato waliuawa kwa kipindi
cha mwaka 2008-2015,ambao ni Lwegamoyo Kilanga mkazi wa kijiji cha Chigunga
alikatwa mkono,Zawadi Magundu mkazi wa Nyamaruru alikatwa miguu na mkono mmoja
na Gaspali Elikana alikatwa mguu wake wa mmoja.
Alisema kuwa
waliojeruhiwa mpaka sasa katika wilaya ya GeitaBibiana Mbushi aliyekatwa mguu wa kulia na vidole viwilii vya mkono,Nelick Elias(4)mkazi wa kijiji
cha Kaseni alinyolewa nywele zote za kichwani kwa ktumia wembe na Adam
Robert(12) mkazi wa nyaruguguna wilaya ya
Nyang’whwale alijeruhiwa mkono wa
kushoto na kukatwa vidole vya mkono wa kulia vyote.
Katika
matukio yote hayo ,ni tukio moja tu la Zawadi Magindu ambalo watu waliofanya
tukio hilo walichukuliwa hatua 5 machi
mwaka huu kwa kuhukumiwa kunyongwa na ni baada ya watu kupiga kelele juu ya
kifo cha mtoto Yohana Bahati.
Timoth
alisema hajalidhika na utendaji wa jeshi la polisi na serikali kwa ujumla
katika kufatilia matukio ya kuuawa ,kutekwa na kukatwa viungo kwa Albino.
“nashindwa
kuelewa hivi karibuni majambazi yalivamia kituo cha polisi Bukombe,tuliona
jinsi serikali na Jeshi la Polisi lilivyofanya kazi hadi majambazi na siraha
zilizoporwa kupatikana lakini unapozungumzia albino wanachukulia mambo
kilahisi”alisema.
Alisema kwa
mantiki hiyo inaoneka thamani ya albino inazidiwa na thamani ya Bunduki.
Jeshi la Polisi linatambua tukio hilo?.
Nilikutana
na Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Peter Kakamba namtonya juu ya
tukio hilo na kutaka kuja kama kuna watu ambao wameshakamtwa au la,lakini
anaonekana kutokulifahamu kabisa,ndipo aliponikbidhi kwa Ofisa Upelelezi wa
makosa ya jinai mkoa Peter Kayumba.
Ofisa huyo
anaomba nimpe muda ili afatilie kujua kama kunatukio la aina hiyo.
“Naomba nifatilie,maana
sisi nimgeni ili nijue kama kunatukio la aina hiyo na ikiwezekana niende kwenye
hizo familia”alisema Kayumba.
Gerald Ruhele
ni Mkurugenzi wa mtandao wa Mashirika
yasiyoyakiserikali yanayotetea haki za binadamu mkoani Geita yeye anasema
analifahamu tukio hilo na kwamba walishatoa taarifa kwa vyombo vya dora na
serikali hivi karibuni ili kulifatilia.
“Tunafahamu
tukio hilo sisi kama mtandao wa mashirika yasiyoyakiserikali na linatuumiza
sana,tumeandaa warsha mwezi huu utakao husisha wadau wote na tuki hilo
tutalipigia kelele ili waliohusika wachukuliwe hatua”alisema.
Mwisho
Wananchi mkoa wa Geita wakiwa katika matembezi ya amani ya kupinga mauaji ya Albino yaliyofanyia Februari 27 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment